Overblog
Editer l'article Suivre ce blog Administration + Créer mon blog
La Tribune franco-rwandaise
Actualités, opinions, études, analyses, diplomatie et géopolitique de la Région des Grands lacs.

Tanzania yauwakia Umoja wa Mataifa

JMV Ndagijimana #Diplomatie

Na Jesse Kwayu

30th November 2009


 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe


Tanzania imetaka kuombwa radhi na Umoja wa Mataifa (UN) kutokana na kupakaziwa kwamba inasaidia kutoa silaha kwa waasi wa FDLR waliojichimbia mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakipigana dhidi ya serikali ya nchi hiyo na Rwanda.


Akitoa tamko la Tanzania mbele ya waandishi wa habari mjini hapa juzi usiku, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema taarifa ya UN ambayo imetokana na kikundi cha wataalamu watano wa umoja huo ni ya kihuni na yenye nia ovu dhidi ya Tanzania.

“Tunahitaji kuombwa radhi kwa taarifa hii ambayo inaonyesha wazi kwamba ina nia mbaya dhidi ya Tanzania,” alisema Membe kwenye mkutano huo.


Alisema kwamba Tanzania imepokea habari kwamba inasaidia waasi wa DRC kwa mshituko na kutokuamini kama umoja huo unaweza kuruhusu taarifa ya kihuni kama hiyo ambayo haina ushahidi wowote wa maana wa kina kutolewa dhidi ya taifa ambalo limejitolea kwa nguvu zake zote kutafuta amani ya kudumu katika ukanda wa Maziwa Makuu.

“Taarifa hii moja kwa moja ina nia mbaya na ni uongo uliotungwa kwa nia ovu kuchafua jina zuri la Tanzania na serikali yake,” alisema Membe.


Waziri huyo aliongeza kwamba Tanzania kamwe hajajihusisha wala kuwaza kushiriki katika vitendo viovu vya kuuza silaha haramu kwa nia ya kuchochea uasi kwa nchi yoyote jirani kama Rwanda na DRC.

Alisema kinyume chake, Tanzania inajitoa kwa kadri ya uwezo wake kusaidia kukomesha vitendo vya kueneza migogoro katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu.

Waziri Membe alisema kwa takribani miaka 15 iliyopita rekodi ya Tanzania katika kusaka amani ya eneo la Maziwa Makuu inajidhihirisha yenyewe.

“Kamwe Tanzania haitakuwa ndumilakuwili,” Membe alisisitiza. Alisema tangu kutolewa kwa taarifa hizo, serikali imekuwa inajiuliza sihaha hizo zinatoka wapi, lakini kwa bahati mbaya ripoti yenyewe wala haisemi zinatoka wapi ila inajielekeza tu kutoa maelezo ya kubashiri na kunukuu watu ambao hawatajwi ni akina nani waliotoa maelezo hayo.

“Taarifa ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameiacha Tanzania ikishangaa kwa kiwango cha uzembe na kukosekana kwa ueledi kwa watu waliochaguliwa na Umoja wa Mataifa, taasisi ambayo Tanzania inatambua kama makini na ya kuheshimika. Kwa hali hii tumeachwa bila shaka yoyote kuamini kwamba taarifa hiyo ina nia mbaya dhidi ya Tanzania,” alisema Membe.


Alisisitiza kwamba Tanzania haina duka lolote lionalouza silaha za vita na wala hakuna ruhusa ya kufanya biashara hiyo nchini kwa sasa wala hakuna mipango ya kuruhusu kwa siku za usoni.

Waziri Membe alisema kwa kuwa silaha kama hizo ndani ya Tanzania ziko mikononi mwa Jeshi la ulinzi, kuihusisha Tanzania na silaha haramu maana yake ni kusema kwamba majeshi ya taifa ndiyo yanatoa silaha kwa waasi.


Alisema haijatokea na kamwe haitatokea kwa vyombo vya usalama vya Tanzania kushiriki kutoa silaha zake kwa waasi wa DRC, pia alisisitiza hakuna taarifa za kupotea kwa silaha kutoka maghala ya majeshi ya nchi.

Kutokana na hali hiyo, Tanzania imeitaka Umoja wa Mataifa upuuze ripoti hiyo ya wataalamu na kila mmoja aitazame kuwa ina nia ovu dhidi ya Tanzania na iombwe radhi.


Alisema kwamba Tanzania itaendelea kuwa mwanachama wa UN anayejali wajibu wake na itaendelea na juhudi za kusaka amani ya kudumu katika ukanda wa maziwa makuu.

Alitoa mfano kwamba tangu mwaka 1959 Tanzania imekuwa kimbilio la wakimbizi wanaokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe kutoka nchi za jirani, na uthibitisho wa hivi karibuni ni uamuzi wa Tanzania kutoa uraia kwa wakimbizi 160,000 wa Burundi waliokataa kurejea kwao kwa hiari.


Kadhalika, alikumbusha kwamba kama sehemu ya kusaidia kupatikana kwa amani DRC, Tanzania ilimtoa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, akishirikiana na Rais Mstaafu wa Nigeria, Jenerali Olusegun Obasanjo, kusaidia kupatikana kwa amani ya nchi hiyo kazi aliyoanza Januari 18, mwaka huu na sekretariati yake imekwisha kulipiwa na Tanzania Dola za Marekani 500,000 kufanikisha kazi hiyo.

 

CHANZO: NIPASHE

 

Pour être informé des derniers articles, inscrivez vous :
Facebook Twitter RSS Contact